Mkoa wa Tanga upo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania kati ya latitudo 4 0 na 6 o Kusini na longitudo 37 o na 39 o Mashariki. Kwa upande wa Kaskazini inapakana na Jamhuri ya Kenya na Kusini inapakana na Mikoa ya Morogoro na Pwani, upande wa Magharibi inapakana na Mikoa ya Manyara na Kilimanjaro na Mashariki inapakana na bahari ya Hindi na visiwa vya Unguja na Pemba.
Mkoa wa Tanga una eneo la kilomita za mraba 26,809 sawa na asilimia 3.03 ya eneo la Tanzania Bara. Eneo la Pwani linalojumuisha ghuba na milango ya mito ni zaidi ya kilomita 407 za urefu wa ufukwe wa mwambao wa bahari ya Hindi na upana wa Kilomita za mraba 2,090 zilizopo kati ya kilomita 5 na 40 za eneo la uvuvi (Continental shelf) ambapo kuna jumla ya miamba ya matumbawe 96 na fukwe zina jumla ya hekta 15,966 za misitu ya mikoko.
Mkoa umegawanyika katika Wilaya 8 zenye Halmashauri 9, Tarafa 37, Kata 158, Vijiji 714, Mitaa 85 na Vitongoji 4218.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002, idadi ya watu ilikuwa ni 1,636,280 (wanaume 793,159 na wanawake 843,121), kukiwa na wastani wa ongezeko la watu la asilimia 1.8 kwa mwaka. Kwa ongezeko hili, mwaka 2012 Mkoa unakadiriwa kuwa na watu 2,054,042. Wastani wa msongamano wa watu (Population Density) kwa mwaka 2002 ilikuwa watu 61 na mwaka 2012 inakadiriwa kuwa watu 76.6 kwa kilometa za mraba. Msongamano huo ni mkubwa katika Wilaya ya Tanga (512), Mji Korogwe (255) na Lushoto (120) huku Wilaya ya Pangani ikiwa na msongamano mdogo kuliko Wilaya zingine kwa watu 30.8 kwa kilometa za mraba.