Ujenzi huo umeanzishwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika sherehe ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho kitakachoanza uzalishaji Oktoba, 2010,
na kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 4,000 kwa siku. Ujenzi huo utachukua miezi 24.
Kiwanda hicho kinajengwa na Kampuni ya Athi River Mining Ltd (ARM) yenye makao yake nchini Kenya, na kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi kuliko kingine chochote cha uzalishaji saruji katika eneo la Mashariki mwa Afrika kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,500,000 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Pradeep Paunrana amemwambia Rais Kikwete kwenye sherehe hiyo:
“Kupitia uzalishaji huu wa tani 4,000 kwa siku, tunapenda kukuhakikishia kwamba uhaba wa saruji litakuwa ni historia, bei zitakuwa za ushindani na zitakuwa bei halisi badala ya bei za sasa za saruji zinazoongozwa na uhaba wa bidhaa hiyo.”
Mkurugenzi huyo amesema kuwa kampuni yake ambayo imekuwa na shughuli nchini kwa miaka sita iliyopita, imevutiwa kuwekeza zaidi katika uchumi wa Tanzania kutokana na kugundua mvuto wa uchumi huo.
“Mheshimiwa Rais, baada ya kuwa tumeonja utamu wa uchumi wa Tanzania, na maisha yanayozidi kuwa bora kila siku kwa kila Mtanzania, lilikuwa ni jambo la dhahiri kabisa kuingia katika uzalishaji wa saruji hapa nchini,” amesema Praunrana.
ARM ambacho kwa miaka sita iliyopita imekuwa inazalisha chokaa inayotumiwa katika uchimbaji madini nchini, inazalisha bidhaa za viwandani katika Afrika Kusini, Zambia na Kenya, ambapo kampuni hiyo pia inazalisha saruji.
Mkurugenzi huyo amemwambia Rais Kikwete kuwa ARM imeamua kuwa uzalishaji wote wa siku ya kwanza Oktoba 2010, yaani tani 4,000 ama malori 125 ya saruji, itatolewa yote kwa Rais Kikwete ambaye ataamua kuitumia atakavyo kwa miradi ya kijamii aitakayo.
Kiwanda hicho kipya kitaifanya Tanzania kuwa nchi pekee katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika kuwa na viwanda vinne vya saruji.
Viwanda vitatu vilivyoko kwa sasa ni Tanzania Portland Cement Company (TPCC) ama Twiga Cement cha Dar Es Salaam, Simba Cement cha Tanga na Mbeya Cement cha Mbeya.
TPCC ndiyo kiwanda cha kwanza cha saruji Tanzania kilichofunguliwa Agosti 8, mwaka 1966 na Baba wa Taifa, Mwalimu JK Nyerere.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo Rais Kikwete ameipongeza ARM kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika uzalishaji wa saruji ambao sasa utaiwezesha Tanzania kuzalisha tani 3,000,000 kwa mwaka baada ya kuwa kiwanda hicho kimekamilika katika miaka miwili ijayo.
Pamoja na kwamba uzalishaji saruji nchini umekuwa unaongezeka, bado uwiano wa saruji na idadi ya wananchi wa Tanzania umebakia ndogo.
Amesema kuwa mwaka 2005 wakati wananchi wa Tanzania wanakadiriwa kufikia milioni 37, matumizi ya saruji yalikuwa sawa na kilo 37 kwa kila Mtanzania kwa mwaka.
“Matumizi haya bado ni madogo ikilinganishwa na matumizi ya saruji nchini Kenya ambayo ni wastani wa kilo 56 kwa mtu mmoja kwa mwaka. Nchini Afrika Kusini, matumizi haya yanafikia wastani wa kilo 400 kwa mtu mmoja kwa mwaka.” |