Na Mashaka Mgeta, MKINGA
WASWAHILI wanasema, ’mali bila daftari, hupotea bila habari.’ Lakini kwa Monica Kigoda, mkazi wa kijiji cha Duga Maforoni wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, hali si hivyo.
Monica ametembelewa na Mwenge wa Uhuru 2025 leo Juni 15, 2025 kwenye eneo la mradi wa ufugaji kuku, akasimulia sehemu ya historia ya maisha yake tangu kuanza kwa biashara hiyo hadi sasa.
Akiwasilisha taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi, Monica amesema alianza biashara ya ufugaji kuku mwaka 2018 akiwa na mtaji wa Shilingi 300,000 iliyotokana na uuzaji wa mazao ya kilimo cha bustani, ambapo alinunua vifaranga, dawa na chakula.
Akiwa amesimama mbele ya Mwenge wa Uhuru wenye ujumbe unaosema, JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU, Monica akasema biashara hiyo ilikuwa hatua kwa hatua, na kwa kufuata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa Maafisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, mtaji wake umekua hatua kwa hatua.
Monica anasema ukuaji wa mtaji umekuwa pamoja na ongezeko la idadi ya kuku anaowafuga, akitoa mfano kuwa alianza na kuku 100 , idadi hiyo ikaongezeka kufikia 800..
Kiongozi wa Mbio wa Mwenge wa Uhuru 20205, Ismail Ali Ussi, anasema Monica ni mfano wa kuigwa kwa uthubutu na ukuzaji wa biashara, hivyo anapaswa kuungwa mkono na wadau katika sekta za umma na binafsi.
Ussi amesema simulizi za Monica zimeonesha mapito ya ’milima na mabonde’, lakini akavumilia changamoto na sasa amekuwa na hadhi ya kufikiwa na Mwenge wa Uhuru 2025.
Kwa mujibu wa Ussi, vijana wanapaswa kutambua kuwa kazi za uzalishaji, huduma na ujasiriamali wanazoshiriki, zinathaminiwa sana nchini, kwa vile ni sehemu ya kutekeleza mang’amuzi ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania kujitegemea na kuboresha maisha yao.
Ussi amesema hatua ya Monica kuwaajiri wakazi wengine wa Mkinga kushiriki biashara yake ya ufugaji kuku, ni sehemu ya uungwaji mkono na kumpa heshima Mhe Rais Dkt Samia.
”Monica, ulijitoa sana wakati ukinzisha ufugaji kuku kutokea nyumbani kwako, umestahimili changamoto nyingi ambazo sasa zinaondoka na unakuwa mwenye kuheshimika zaidi katika jamii yetu,” amesema Ussi.
Kiongozi wa Mwenge huyo, amesema itafaa sana ikiwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga itamuendeleza Monica kupitia mafunzo ya ndani na nje ya nchi, ili aweze kusambaza stadi za ufugajji kuku kwa Watanzania wengi zaidi.
.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.