DK MPANGO: MITAMBO MIWILI YA JNHPP KUWASHWA MWEZI UJAO
Na Mashaka Mgeta na Zuberi Mgaya, HANDENI
MAKAMU wa Rais, Mhe Dk Philip Mpango, amesema mitambo miwili iliyopo kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), itawashwa mwezi ujao wa Machi mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na upungufu wa nishati hiyo nchini.
Mhe Dk Mpango amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Handeni kwenye eneo la Kabuku, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu mkoani Tanga.
Kauli ya Mhe Dk Mpango ilitanguliwa na hoja ya Diwani wa Kata ya Kabuku Ndani wilayani Handeni, Mhe Abdallah Pendeza, kuainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo ikiwemo mgawo wa umeme.
Mhe Dk Mpango amesema, awali, Serikali inayotekeleza mipango ya kitaifa na inayohusu maeneo mahususi kukabiliana na upungufu wa umeme, ilipanga kuwasha mtambo mmoja kuongeza umeme kwenye gridi ya taifa, lakini iliahirishwa na badala yake itawashwa mitambo miwili mwezi ujao.
Kuhusu hatua mahususi za kupunguza changamoto ya hiyo kwenye baadhi ya maeneo mkoani Tanga, Mhe Dk Mpango amesema Serikali inajenga kituo cha kupozesha umeme katika kata ya Mkata wilayani Handeni, hivyo wananchi wanatakiwa kuwa na subira wakati mradi huo ukitekelezwa.
Mhe Dk Mpango, ameagiza kukamilika haraka kwa ujenzi wa kituo cha afya cha Kabuku, ili kuendeleza jitihada za Serikali ya Rais Mhe Dk Samia Suluhu Hassan, kuboresha afya za wananchi wake.
Naye Meneja wa TANESCO katika wilaya ya Handeni, Mwalimu Mussa Kassim, baada ya kuruhusiwa na Mhe Dk Mpango, akasema vijini 91 na mitaa 60 iliyopo wilayani humo imefikiwa na huduma ya umeme na kwamba vitongoji 250 kati ya 770 vilivyopo halmashauri ya wilaya hiyo ndivyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme.
Mwalimu Kassim amemhakikishia Mhe Dk Mipango kuwa vitongoji hivyo vitafikiwa na huduma hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.