Na Mashaka Mgeta, MUHEZA
VIJIJI vitano vya wilayani Muheza katika Mkoa wa Tanga, yaani Kibanda, Mkinga, Tingeni, Mindu na Mbambata, vimekuwa kwenye kadhia ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu.
Lakini sasa kero inaondoka, ikiwa ni ishara ya kufutika kwa historia ya ukosefu wa maji safi na salama, kufuatia visima virefu vinavyojengwa kwenye vijiji hivyo.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Muheza, Mhandisi Omary Mohamed, amesema hayo wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tanga, ilipotembelea na kukagua miundombinu ya chanzo cha maji ya mradi huo kilichopo kijijini Mkinga.
Mhandisi Mohamed amesema ujenzi wa visima hivyo unaotarajiwa kukamilika Juni 30, mwaka huu, unatekelezwa kupitia kampuni za JNB Construction na Frangem International Limited.
Amesema mradi huo utagharimu Shilingi milioni 291.1, huku ukiwahudumia wakazi 3,950 waliopo kwenye maeneo ya mradi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mohamed, chanzo hicho kina urefu wa mita 160 kilichochimbwa majira ya kiangazi, kikiwa na uwezo wa kutoa lita mbili za maji kwa sekunde moja.
Amesema kutokana na uwezo huo, inachukua saa tano pekee kujaza tenki lililopo kwenye chanzo hicho, likiwa na ukubwa wa lita za ujazo 10,000 na uwezo wa kuwahudumiwa watu 800 kwa wakati mmoja.
Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Mfaume Kizigo, ametoa rai kwa watendaji hasa katika ngazi za Serikali za Mitaa, kutumia vyombo vya habari kuujulisha umma mpana kuhusu miradi iliyopo kwenye maeneo yao na manufaa kwa maisha yao.
Amesema zipo habari njema nyingi zinazohusu utekelezaji wa miradi na maendeleo kwenye maeneo tofauti na ambazo haziifikii jamii ipasavyo, kutokana na ushirikishwaji mdogo wa waandishi na vyombo vya habari.
Kizigo amesema, pamoja na ukweli upataji habari zilizo sahihi na kweli ni haki ya kila raia, lakini hali hiyo inachochewa zaidi ya uwepo wa taarifa zinazohusu sekta zenye ‘kugusa’ maisha ya walio wengi.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.