Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
IDARA za Rasilimaliwatu na Sheria katika sekta ya umma, zinahusika kwa sehemu kubwa na masuala ya nidhamu za watumishi na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi.
Lakini, kama ilivyo kwa taasisi nyingine, idara hizo zinakabiliwa na changamoto tofauti, ikiwemo uelewa mdogo wa mamlaka za nidhamu kwa majukumu yao ipasavyo, hivyo kusababisha watumishi wa umma kukiuka maadili ya kazi.
Katibu Mkuu Ikulu, Mululi Mahendeka, ameielezea hali hiyo jana Mei 19, 2025, alipofungua mafunzo kuhusu sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema.
Mahendeka anasema uelewa wa majukumu ya mamlaka za nidhamu una athari kubwa katika kuzuia ama kushughulikia malalamiko na rufaa nyingi za mashauri ya nidhamu katika ngazi za juu za uongozi, zinazotokana na maamuzi yasiyozingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo.
Amesema, usimamizi mzuri wa maadili na nidhamu kwa watumishi wa umma, na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi kwa ufanisi, unawezesha Serikali kufikia malengo yake ikiwa ni pamoja na kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Pia, amesema hali hiyo itasaidia kuwa na watumishi waadilifu, wawajibikaji, wanaofanya kazi kwa uwazi na wanaotumia vizuri rasilimali zilizopo.
Mahendeka amesema, watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano kwa uadilifu na uwajibikaji kwa wengine, kama anavyoelekeza mara kadhaa, Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akihimiza uwepo wa nidhamu hasa wanapohudumia wananchi.
“Maneno ya Kiongozi wetu ni maelekezo na yanadhihirisha kuwa hapendi kuona watumishi wa umma tunashindwa wajibu wetu, hivyo tunatakiwa kuongeza ufanisi wa kazi na kuondoa malalamiko na kero kwa wananchi,” amesema.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.