Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KATIBU Mkuu Ikulu, Mululi Mahendeka, amewataka watumishi wa umma kuzisoma, kuzielewa na kuzistafisiri kwa vitendo sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali, ili kufanikisha utoaji huduma unaokidhi utatuzi wa kero za wananchi.
Mahendeka ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tano yaliyoanza leo Mei 19, 2025 mjini hapa, yakiwashirikisha watumishi wa Idara za Rasilimaliwatu na Sheria kutoka taasisi 23 za Serikali, wanaohusika na masuala ya nidhamu za watumishi na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi.
Lengo la mafunzo hayo ni kukumbushana na kueleweshana uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi, hasa kwenye usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya nidhamu, malalamiko, rufaa na kero za watumishi na wananchi wengine.
Hotuba yake kwenye mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Ikulu kwa kushirikisha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Tume ya Utumishi wa Umma, imesomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema.
Mahendeka amesema, kwa kufanya hivyo jamii itanufaika kwa usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya nidhamu, malalamiko, rufaa na kero za watumishi wa umma na wananchi kufanyika kwa haraka, ukamilifu na kupatiwa ufumbuzi.
Pili ni kuwaondolea wananchi na watumishi wa umma usumbufu wa kufuatilia majibu ya malalamiko, kero kwenye mamlaka za juu kama vile kwa Mhe Rais, Mhe Makamu wa Rais, Mhe Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi na viongozi wengineo.
Tatu, kuepuka gharama ambazo Serikali inaweza kulipa, endapo imeshindwa kesi inayotokana na suala la hatua za kinidhamu, zilizochukuliwa kwa mtumishi wa umma au mwenye madai dhidi ya Serikali.
Nne, kuepusha wananchi wakiwemo watumishi wa Serikali, kuichukia Serikali pale ambapo hawakuhudumiwa vizuri au malalamiko, kero zao hazikutatuliwa kwa wakati.
Kero za wananchi ama watumishi zinapofanyiwa kazi kwa haraka na wakati, zinafanya waiamini zaidi Serikali na kushiriki ipasavyo katika shughuli za maendeleo.
Tano, kuepusha viongozi wakuu wa nchi kutumia muda mwingi kusikiliza malalamiko, kero za wananchi na kuzitatua, wakaati wana majukumu mengi kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.