Na Mashaka Mgeta, OMM-TANGA
UPO usemi unaosema, ‘’mtu anapofanya jambo la kusifiwa, sharti asifiwe’’. Ndivyo inavyotamkwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe Hashim Mgandilwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian.
Mhe Mgandilwa anayesema hayo kufuatia ‘kuguswa’ na mafanikio ya mkoa huo katika sekta ya elimu na ukusanyaji mapato ya ndani, kwamba vimechochewa na usimamizi, ufuatiliaji na maelekezo ya Mhe Balozi Dk Batilda.
Anasema hayo leo Julai 16, 2024, baada ya Mhe Balozi Dk Batilda, kuelezea furaha yake kwa matokeo mazuri katika sekta hizo.
Akizungumza kwenye halfa ya kukabidhi magari manne kwa Wakuu wa Wilaya tatu na Mkuu wa Idara ya Mipango katika Sekretarieti ya Mkoa huo, Mhe Balozi Dk Batilda, amesema matokeo ya kidato cha sita yanayoonesha mkoa huo kujitokeza kwenye ‘kumi bora’, kunatia moyo wa kuzidi kukuza kiu ya kuiboresha zaidi sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Mhe Balozi Dk Burian, Shule ya Sekondari ya Mkindi na wasichana waliofanya vizuri kwenye ‘kumi bora’ kitaifa, ni ishara kwamba upo uwezekano kwa mkoa huo kufanya vizuri zaidi kwenye maeneo hayo.
‘’Kwa vile historia inaonyesha hapa Tanga ndipo elimu ilipoanzia nchini, hatujaridhika na mafanikio ya mwaka huu, tunajipanga kufanya vizuri zaidi,’’ amesema.
Mhe Balozi Dk Burian amesema, pamoja na mafanikio hayo, jitihada za uboreshaji wa sekta ya elimu, unachochewa pia na hatua ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kuwekeza fedha nyingi mkoani humo.
Amesema miongoni mwa fedha hizo ni Shilingi bilioni 3 zilizotumika kujenga Shule Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga iliyopo Mabalanga wilayani Kilindi, sasa imewapokea kwa mara ya kwanza wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu.
Mhe Balozi Dk Burian amesema, serikali imetoa fedha nyingine, Shilingi bilioni 1.1 kuendeleza ujenzi wa miundombinu shuleni hapo.
Mhe Balozi Dk Burian, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe Mgandilwa kuongeza ufuatiliaji, usimamizi na ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo.
Kuhusu mapato ya ndani kwa mwaka 2023/2024, Mhe Balozi Batilda amesema hatua ya kufikia asilimia 104 inaonesha uwezekano wa kukusanya mapato zaidi mkoani humo.
Takwimu za makusanyo hayo na asilimia ya malengo kwa kila halmashauri kwenye mabano ni Kilindi (131), Mji Handeni (128), halmashauri ya wilaya Handeni (125), Muheza (108) na Bumburi (102).
Halmashauri nyingine ni jiji la Tanga, Mkinga na Lushoto zilizofikisha asilimia 98 kila moja, halmashauri ya wilaya Korogwe (97), Mji Korogwe (93) na Pangani (95).
Hapo ndipo Mhe Mgandilwa anasema, mafanikio hayo hayawezi kuweka kando nafasi ya maelekezo, ufuatiliaji na usimamizi wa Mhe Balozi Dk Burian, kupitia Sekretarieti ya Mkoa inayoongozwa na Katibu Tawala Mkoa, Pili Mnyema.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.