Na Mashaka Mgeta, OMM - TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amewaagiza watumishi wa sekta ya maji mkoani humo, wasiwe chanzo cha changamoto ama vikwazo katika mipango wa kufikisha huduma hiyo kwa wananchi.
Mhe Balozi Dk Burian, amesema hayo leo Julai 2, 2024, wakati akifunga mafunzo ya Uunganishaji wa Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSO) kwenye mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato, yaliyofanyika kwa siku 15 mkoani hapa.
Amesema sekta ya maji ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kupitia nadharia ya ‘kumtua mama ndoo kichwani’, hivyo watumishi hao wanapaswa kujikita katika utoaji huduma na usimamizi usiokuwa na vikwazo ama kuibua, badala ya kudhibiti changamoto kwenye sekta hiyo.
Pia Mhe Balozi Dk Batilda ameelezea kuridhishwa na mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato na kwamba utachangia kuongeza makusanyo ya Serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema, amewataka watumishi wa umma na wafanyakazi kwenye CBWSO 46 za mkoani humo, kuwa waelekezaji wema kwa wananchi katika kutumia mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki.
‘’Mnapokwenda kusimamia utekelezaji wa makusanyo ya mapato kwa kutumia njia hii mpya ya kielektroniki, muwe waelekezaji na sehemu ya kutoa majawabu sahihi kwa watu wanapohitaji kujua zaidi,’’ amesema.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo amesema, matumizi ya mfumo huo yaliyoanza Juni 30, 2024 yamewezesha ukusanyaji wa Shilingi milioni saba ndani ya siku mbili pekee.
Mhandisi Upendo amesema kupitia fedha hizo zilizo sehemu ya makusanyo ya serikali yanafanyika kwa njia rahisi ya kutumia mitandao ya simu za mkononi ama wakala wa benki.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.