Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Mhe Zubeir Ali Maulid leo Aprili 25, 2025 ametembelea miradi ya maendeleo katika sekta za elimu na uchumi, yenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 7.4 mkoani Tanga.
Mhe Maulid yupo mkoani humo kwa ziara ya siku nne iliyoanza jana, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa Aprili 26, 1964.
Mradi wa kwanza ulikuwa ujenzi wa madarasa manne ya kidato cha tano na sit ana matundu saba ya vyoo kwenye Shule ya Sekondari Bushiri wilayani Pangani ulioanza Januari 25, 2024 na kugharimu Shilingi milioni 116.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Charles Fussi, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne kupata nafasi zaidi za kujiunga kidato cha tano, na kuongeza hamasa ya kuthamini elimu.
Aidha, Mhe Maulid alitembelea mradi wa ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Zingibari wilayani Mkinga, unaogharimu Shilingi milioni 260.
Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Omar Rashid, amesema mradi huo uliibuliwa ili kutatua changamoto ya upungufu wa mabweni kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kuisaidia jamii ya wanafunzi kuwa salama na kuongeza ufaulu.
Pia Mhe Maulid, ametembea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya soko la wafanyabiashara wadogo kwenye eneo la Kange jijini Tanga ambao hadi kukamilika kwake, utakaogharimu Shilingi bilioni 7.7.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Gwakisa Lusajo amesema ujenzi wa soko hilo utafanyika kwa awamu nne na inakisiwa, kila awamu itagharimu Shilingi bilioni 1.9, lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara wadogo.
Spika wa BWZ, Mhe Maulid amesema miradi hiyo na mingine iliyopo sehemu nyingine za mkoa huo na nchini, ni sehemu ya vilelezo vya namna Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, inavyotekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020 hadi 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Dkt Batilda Burian, amesema ufanisi katika utekelezaji wa miradi mkoani humo, unachochewa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali, Chama tawala na wananchi.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.