Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
WATUMISHI wa sekta ya umma katika mkoa wa Tanga, leo Julai 13, 2024 wameshiriki mbio fupi za asubuhi kwa pamoja ili kuimarisha afya zao, ushirikiano na kuzindua mazoezi kwa ajili ya ushiriki kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
Mbio fupi hizo zimefanyika kwa umbali wa maili 3.18, sawa na kilomita 5.12 huku zikichukua dakika 46 na wastani wa mwendo wa dakika moja kwa kimomita 0.03.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema, amesema pamoja na kuzindua safari ya kuelekea SHIMIWI 2024, mbio za leo zililenga kuwakutanisha watumishi wa umma katika mpango wa kuboresha afya zao kwa njia ya mazoezi.
Kwenye hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Afisa Michezo Mkoa wa Tanga, Digna Tesha, Katibu Tawala Mkoa huyo amesema mazoezi yanapaswa kuwa jambo endelevu kwa watumishi wa umma na Watanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mnyema, mazoezi ya timu ya Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga na taasisi zilizo chini yake, yatafanyikia kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga, kabla ya kuekelea mkoani Morogoro Septemba mwaka huu kushiriki SHIMIWI.
Mnyema amesema michezo ni jambo muhimu na kwamba, licha ya kuwaweka imara kimwili, watumishi wa umma wanatumia fursa hiyo kwa ajili ya kuimarisha mahusiano sehemu za kazi.
Amewahimiza wananchi mkoani Tanga kuendeleza hulka ya kufanya mazoezi bila kusubiri matukio mahususi, kwani kufanya hivyo itawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.
Mnyema amesema mbio fupi za asubihi ya leo zimeshirikisha taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, vikundi vya jogging kama vile Tanga Uwasa, shule za sekondari Galanosi na Usagara, Mkwakwani, Tanga Kwanza, Bomboka,Tanga Raha na Wakfu wa Aweso kutoka Pangani.
Naye mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Edna Msumi amesema, watumishi wa afya wanatambua kuwa michezo ibaboresha afya za watu na kuchagiza mahusiano mema.
Mmoja wa washiriki kwenye mbio hizo, Christopher Mnkabenga kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga, amesema uzinduzi wa leo umewapa ari ya kujiandaa na ‘mazoezi mzito’ kwenda kutwaa ushindi kwenye michezo mbalimbali inayoshindaniwa SHIMIWI.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.