Na Mwandishi Wetu OMM TANGA
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewaasa Waandishi wa Habari kuzielewa, kuzitetea na kuzieneza haki za binadamu kupitia utekelezaji wa majukumu yao katika kuhabarisha na kuielimisha jamii.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Utafiti na Nyaraka wa THBUB, Monica Mnanka, ameyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya Waandishi wa Habari mkoani Tanga kuhusu masuala ya haki za binadamu hususani wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Kwa kutambua mchango na umuhimu wa waandishi wa habari katika uchaguzi, Monica amesema THBUB itatoa elimu ya uraia kwa Waandishi wa Habari na kufanya ufuatiliaji wa uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora wakati wa uchaguzi katika mikoa 13 ya Tanzania Bara na mitano ya Zanzibar.
Katika muktadha wa uchaguzi ulio wa huru, haki na wenye kuzingatia misingi ya demokrasia, Monica amesema vyombo vya habari vina nafasi katika upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma kwa vile ni daraja kati ya wagombea, vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wananchi.
Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinachangia kujenga uelewa wa wapiga kura kuhusu sera na ajenda za kisiasa, kuhamasisha ushiriki wa wananchi na kuchochea uwajibikaji wa kisiasa ili kudumisha amani na demokrasia katika kipindi chote cha uchaguzi.
Pia, Monica amewaasa Waandishi wa Habari kuepuka matumizi ya lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji, rushwa, takrima, vitisho zawadi zenye lengo la kushawishi maudhui yenye kuegemea upande wa chama ama mgombea fulani katika kuripoti matukio ya uchaguzi.
Maeneo mengine ambayo Monica ameasa kuepukwa ni kuchapisha au kutangaza habari zenye nia ya kuchochea vurugu, ubaguzi au chuki za kisiasa, kikabila, kidini, kijinsia na kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.
Naye Afisa Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Tanga, Mashaka Mgeta, amesema kiwango cha uhuru na haki ya waandishi kutekeleza majukumu yao ikiwemo katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu ni kikubwa ikilinganishwa na maeneo mengine ya ndani na nje ya ukanda wa Afrika.
Kwa hali hiyo, amesema Waandishi wa Habari wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Misingi ya uandishi wa habari ili kutekeleza majukumu yao kwa maslahi mapana ya nchi na watu wake.
Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Tanga, Herman Mbonea, ameishukuru THBUB kuwatambua wadau wa haki za binadamu wakiwemo Polisi na Waandishi wa Habari, ili kufanikisha azma ya kuzifanya haki za binadamu zizidi kutamalaki nchini.
Kwa mujibu wa tovuti ya THBUB, Tume hiyo ni idara huru ya Serikali, iliyoanzishwa kama taasisi ya kitaifa iliyo kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini
THBUB ilianzishwa chini ya Ibara ya 129(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 3 ya mwaka 2000.
Tume ilianza kazi Julai 1, 2001 baada ya kuanza kutumika kwa Sheria ya THBUB Sura ya 391 na Tangazo la Serikali Na. 311 la Juni 8, 2001 na ilizinduliwa rasmi Machi 15, 2002 baada ya kuteuliwa na kuapishwa kwa Makamishna wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Tume ilianza kazi rasmi Aprili 30, 2007 baada ya Sheria ya THBUB Sura ya 391 kuridhiwa na Baraza la Wawakilishi kwa kutungiwa Sheria Na. 12 (Extension Act) ya Mwaka 2003.
Kwa kuzingatia Ibara ya 130(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 6(1)(a) na (d) cha Sheria ya THBUB, Sura ya 391 ya Sheria za Tanzania, Tume ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii, kufanya utafiti, kutoa na kueneza nchini elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.